Story
Ni wangapi kati yetu wanaosimama na kuwaambia wengine yale wanayoyaamini kuhusu Yesu Kristo? Ni wangapi kati yetu wenye hakika kweli kwamba imani yetu imekuwa sehemu kamili ya utu wetu hata inastahili kuitangaza kwa furaha kwa wale wanaotuuliza? Kuwa mmoja wa wanafunzi wa Yesu si jambo jepesi, kwa maana Yesu alisema wakati mmoja: "Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani... Nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa... Msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema au mtakayosema... Maana mtapewa saa ile ile mtakayosema...
Nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho ndiye atakayeokoka." (Mathayo 10:16 na kuendelea (Matthew 10:16)) Karibu na mwisho wa karne ya tatu, aliishi mtu wa Kikristo aliyeitwa Marko. Alikuwa mtawala wa wilaya za Borolos na Zaafaran nchini Misri. Marko alikuwa na binti mmoja tu aliyeitwa Demiana. Uzuri wake na tabia yake njema vilikuwa maarufu sana. Baba yake alimpenda mno, naye alifanya jitihada zake zote kumlea katika njia ya Kikristo ya kweli. Demiana alipenda kusali na kusoma vitabu vitakatifu katika faragha ya chumba chake.
Mara nyingi alilia akiwa anasali, kwa kuwa alihisi upendo wa Mwokozi wake Kristo ukijaza moyo wake mdogo. Demiana alipofikia umri wa kuolewa, baba yake alitaka aolewe na mmoja wa rafiki zake watukufu, lakini Demiana alikataa. Alisema kwamba alikuwa amejitoa mwenyewe kuwa bibi arusi wa Kristo, na kwamba alikusudia kuishi bila ndoa maisha yake yote, ili apate kumtumikia Bwana Yesu Kristo. Demiana pia alimwomba baba yake amjengee nyumba kwenye viunga vya mji, ili aishi humo, pamoja na rafiki zake, kama mtawa mbali na ulimwengu na majaribu yake.
Akijua hamu yake kuu ya maisha ya haki, baba yake alimkubalia Demiana ombi lake kwa kusitasita, naye akamjengea kasri kubwa. Demiana akakigeuza kasri hicho kuwa nyumba ya watawa, naye akaishi humo pamoja na rafiki zake arobaini. Wote walikuwa wasichana wasioolewa, na mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, ukiwapa nguvu na faraja. Wakati huo Dioklitiani, Kaisari, alianza kuwatesa na kuwaua Wakristo waliokataa kuabudu sanamu zake (Apolo na Artemi). Marko alipoalikwa kupiga magoti mbele ya vinyago na kutoa uvumba, alikataa. Lakini Dioklitiani alimshawishi kwa kumwahidi kumpa cheo cha juu zaidi katika Milki ya Kirumi.
Demiana aliposikia kwamba baba yake amepiga magoti mbele ya sanamu, aliacha kasri na kwenda kwake mara moja. Akamwambia, "Umewezaje kumkana Mwokozi wako aliyemwaga damu yake kukuokoa, na kupiga magoti mbele ya sanamu za mawe zinazokaliwa na shetani? Ulilofanya, baba yangu, ni woga na aibu." Marko aliposikia maneno ya binti yake, alirudiwa na fahamu zake. Akasema, "Ole wangu, nimewezaje kuangukia mtego wa Ibilisi na kuabudu vile vinyago visivyofaa kitu." Kisha aliinuka mara moja, akaenda kwa Dioklitiani.
Akajifanyia ishara ya msalaba kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu mbele ya watu wote, na kupaza sauti kwa sauti kuu, "Kila mtu na ajue kwamba mimi namwabudu Mungu wa mbingu na nchi, Mungu wangu wa pekee na Bwana wangu Yesu Kristo." Dioklitiani alifadhaika na kujitahidi sana kubadili nia ya Marko, lakini wakati huu Roho Mtakatifu alikuwa amejaza moyo wake, naye akashuhudia kwa ujasiri zaidi kwamba alikuwa tayari kufa kuliko kumkana Mwokozi wake. Dioklitiani aliingiwa na ghadhabu kali sana, na akawaamuru askari wamuue.
Kaisari alipojua kwamba ni Demiana, binti ya Marko, aliyebadili nia ya baba yake, alimwamuru mmoja wa majemadari wake achukue askari mia moja na kuvamia kasri. "Kwanza, jaribu kumshawishi aabudu sanamu zetu", akasema Dioklitiani. "Lakini akikataa, mtishe, mtese, na hata muue ili awe mfano kwa Wakristo wengine." Demiana alipowaona askari wakikaribia kasri, alimwomba Mungu aiimarishe imani yao hadi kufa.
Kisha akawaambia rafiki zake, "Kama mko tayari kufa kwa ajili ya Yesu mnaweza kubaki, lakini kama hamuwezi kustahimili mateso ya askari, ni afadhali mfanye haraka mtoroke sasa hivi." Wale mabikira arobaini walijibu kwamba hawatapoteza uzima wa milele kwa ajili tu ya kufurahia muda mfupi katika ulimwengu huu mwovu. Yule jemadari alipompasha Demiana ujumbe wa Dioklitiani, alijibu, "Nawezaje kumwacha Bwana na Mungu wangu Yesu Kristo na kuinama mbele ya vinyago vipofu, bubu, na viziwi!
Wewe na Kaisari wako mnapaswa kuona aibu kwa matendo yenu ya fedheha, nami nakuambia kwamba hata ukiniua, imani yangu haitatikisika." Yule jemadari alitahayari sana, akawaamuru askari wamtese Demiana kwa namna mbalimbali za ukatili.
Alipohisi maumivu makali yakipita mwilini mwake, aliinua uso wake juu kuelekea mbinguni, akasali, "Bwana wangu Yesu, Mwana wa Aliye Juu uliyesulibiwa ili kuniokoa, nipe nguvu nistahimili maumivu." Wale mabikira arobaini walikuwa wanatazama na kulia, lakini Demiana akawaambia, "Msilie, dada zangu, Bwana wetu Yesu Kristo aliteswa na kuuawa kwa sababu alitupenda, ingawa hakutenda hata dhambi moja. Itanipasaje mimi kukaribisha kifo kwa jina lake, hasa nikiwa na hakika ya utukufu wa mbinguni unaoningoja!" Baada ya askari kuchoka kumtesa Demiana, walitupa mwili wake uliokuwa karibu kufa gerezani.
Lakini Malaika Mkuu Mikaeli alimtokea, akamgusa kwa mabawa yake ya mbinguni, na kuziponya jeraha zake. Siku iliyofuata, yule jemadari alidhani kwamba alikuwa amekufa, lakini aliposimama mbele yake akiwa na afya kamili alishangaa sana. Baadhi ya watu walipoona yaliyokuwa yametokea, walipiga kelele, "Sisi ni Wakristo. Tunamwamini Mungu wa Demiana. Hatuna Mungu mwingine ila Yesu Kristo." Yule jemadari alizidi kufadhaika, akawaua wote. Mateso ya Demiana yaliendelea kwa njia ya ukatili zaidi kwa siku nyingi, lakini tena na tena Malaika Mkuu Mikaeli alimtokea na kumponya.
Siku ya mwisho kabla ya kufa kwake kishahidi, Bwana wetu Yesu Mwenyewe alimjia na kumwambia, "Jipe moyo, mteule wangu. Nimekuandalia taji ya arusi yako mbinguni. Jina lako litakumbukwa milele kwa kuwa litakuwa sababu ya miujiza mingi, na mahali hapa kanisa kuu litajengwa kuliheshimu jina lako lililobarikiwa." Hatimaye yule jemadari aliwaamuru askari wamkate kichwa Demiana kwa upanga, pamoja na wale mabikira arobaini. Jumla ya watu waliouawa kishahidi pamoja na Demiana ilikuwa karibu mia nne.
Miaka michache baadaye, Mfalme Konstantino (mfalme wa kwanza Mkristo) alipoingia madarakani, alimtuma mama yake Malkia Helena kwenye kasri la Demiana. Helena aliizika miili yote aliyoikuta kwa heshima kubwa. Aliuweka mwili wa Demiana juu ya kitanda cha pembe za ndovu na kuupamba kwa kitani cha hariri, na mahali hapo hapo akajenga kanisa. Mtakatifu Demiana pia ana nyumba kuu ya watawa huko Belkas na makanisa mengi nchini Misri yanabeba jina lake. Sala na baraka za shahidi huyu mkuu, Mtakatifu Demiana, na ziwe nasi sote. Amina